RAUNDI ya tatu ya Ligi Kuu ya
Tanzania bara imehitimishwa Jumapili hii kwa michezo nane kupigwa kwenye
viwanja tofauti.
Jumamosi mabingwa watetezi Azam FC,
walikuwa ugenini kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya kupambana na Tanzania Prisons
na timu hizo zilishindwa kufungana baada ya dakika 90 kukamilika matokeo yakiwa
0-0.
Sare hiyo imeishusha Azam FC hadi
nafasi ya pili ikiwa na pointi saba na kuiacha Mtibwa Sugar ikiongoza ligi hiyo
baada ya kuifunga Mgambo JKT Jumapili kwenye uwanja wa Manungu Complex.
Sare hiyo ya Azam pia imeifanya timu
hiyo kupunguza kasi yake iliyoanza nayo kwa kushinda mechi mbili mfululizo za
awali kwa kuzifunga timu za Polisi Moro mabao 3-1 na kushi ikaifunga Ruvu
Shooting mabao 2-0 mechi zote ikicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam
Complex
Lakini matokeo hayo yameisaidia
Tanzania Prisons kufikisha pointi nne kwani kabla ya mchezo huo ilikuwa na
pointi tatu ilizozipata kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ruvu Shooting
Septemba 20
Lakini wakati mabingwa watetezi Azam
wakipunguzwa kasi kwaupande wao Wekundu wa Msimbazi Simba mambo yaliendelea
kutokuwa shwari baada ya kulazimishwa tena sare ya tatu mfululizo na Stand
United ya Shinyanga pambano ambalo limechezwa kwenye uwanja wa taifa Dar es
Salaam.
Mashabiki wengi wa timu hiyo
walikuwa na matumaini makubwa kwa timu yao kuondoka na pointi zote tatu katika
mchezo huo kufuatia bao la kuongoza lililofungwa na Shabani Kisiga dakika ya 34
lakini vijana wa Stand United,ambao wengi wao walikuwa wanacheza kwa mara ya
kwanza kwenye uwanja huo wa kisasa walipambana na kusawazisha bao hilo dakika
ya 44 kupitia kwa Kheri Mohamed.
Matokeo hayo siyo tu yamewauzunisha
mashabiki lakini pia kocha wake mkuu Mzambia Patrick Phiri,ambaye amesema hayo
ni matokeo mabaya kuyapata tangu alipoanza kuifundisha Simba na wanapaswa
kubadilika na kushinda mechi inayofuata ili kuwa na matumaini ya ubingwa msimu
huu.
“Inaumiza kuona tunapoteza pointi
tisa tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani lakini kibaya zaidi tunapata sare na timu
dhaifu kama Stand United tunapaswa kubadilika kama tunataka ubingwa nafasi
pekee ya sisi kubaki kwenye mbio za ubingwa ni kushinda mechi inayokuja dhidi
ya Yanga kama tukipoteza haitakuwa raisi kuwa mabingwa,”amesema Phiri.
waliendelea kubaki nyumbani uwanja
wa taifa ambapo walicheza na Stand United ya Shinyanga na kule Tanga kwenye
uwanja wa Mkwakwani Coastal Union walikuwa wakipambana na wamakonde Ndanda FC
kutoka mkoani Mtwara.
Mbeya City timu ambayo wiki
iliyopita ilipata udhamini wa Kampuni ya vinywaji baridi ya Coke Cola Jumamosi
ilipata sare ya pili ya bila kufungana na Maafande wa Ruvu Shooting ambao
wanaburuza mkia kwa sasa kwa kuwa na pointi moja baada ya kufungwa mechi mbili
za awali.
Sare hiyo imeifanya Mbeya City
kufikisha pointi tano baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Coastal Union na
kutoka sare ya 0-0 na JKT Ruvu na kuifanya timu hiyo kuwepo nafasi ya nne nyuma
ya Yanga,Azam na Mtibwa Sugar wanaoongoza ligi hivi sasa.
Na mchezo wa mwisho Jumamosi Moro
United ilipambana na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Jamuhuri Morogoro na timu
hizo kugawano pointi kwa kutoka sare ya 0-0.
Matokeo hayo yaliinufaisha Kagera
Sugar kwa kufikisha pointi nne baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 2-0 katika
mchezo uliopita uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam wiki
iliyopita na Polisi ilifikisha poiti mbili baada ya mchezo uliopita kutoka sare
ya 1-1 na Simba kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaa.
Timu zote hizo zilifungwa kwenye
mechi zao za kwanza msimu huu ambapo Polisi ilifungwa na Azam FC mabao 3-1 na
Kagera Sugar ilifungwa bao 1-0 na Mgambo JKT.
Ligi hiyo iliendelea tena Jumapili
kukamilisha mzunguko wake wa tatu kwa kuchezwa michezo miwili kwenye miji ya
Dar es Salaam na Manungu Morogoro
Kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam
Yanga ilicheza na JKT Ruvu na kupata ushindi wa mabao 2-1 ushindi ambao
umeiweka nafasi ya tatu timu hiyo kwa kufikisha pointi sita tatu nyuma ya
vinara Mtibwa Sugar.
Katika mchezo huo Yanga ambayo
ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar iliwachukua dakika 36 kupata
bao la kwanza kupitia kwa beki wake Kelvin Yondani kabla ya kiungo wa kimataifa
Haruna Niyonzima kumalizia la pili dakika ya 74 na kuipa pointi tatu timu yake
JKT Ruvu hawakuwa kwenye kiwango
kizuri katika kipindi cha kwanza lakini walizinduka kipindi cha pili na kufanya
mashambulizi mengi lakini walishindwa kubadili matokeo hayo licha ya kupata bao
moja dakika ya mwisho ya mchezo lililofungwa na Jabir Aziz aliyejiunga na timu
hiyo msimu huu akitokea Azam FC.
Mtibwa Sugar chini ya kocha Mecky
Mexime iliendeleza makali yake msimu huu kwa kuwafunga Mgambo JKT bao 1-0
katika mchezo ambao umefanyika kwenye uwanja wa Manungu Morogoro.
Ushindi huo ni watatu mfululizo kwa
Mtibwa Sugar tangu kuanza kwa msimu huu na umeifanya timu hiyo kufikisha pointi
tisa na kuongoza ligi hiyo ikifuatiwa na Azam yenye pointi saba baada ya
kushinda mechi mbili na kutoka sare mmoja.
Kiujumla timu nyingi msimu huu
zimeonyesha ushindani wa kweli pamoja na kwamba ndiyo kwanza imeanza lakini
mechi zilizo chezwa zimeonyesha namna zilivyojiandaa kutokana na kiwango kizuri
zinacho kionyesha.
Huku nyuma haikuwa rahisi kuona timu
kama Simba ikipata sare kwenye mechi tatu uwanja wa taifa lakini hali hii
inatokana na maandalizi mazuri ya timu ilizokutana nazo lakini pia na ukuaji wa
soka la Tanzania ambao umepiga hatua na siyo kubaki kwa Simba na Yanga.
Ligi hiyo itaendelea tena Oktoba 18
ambapo kutakuwa na michezo mingi ikiwemo ile mechi ya mahasimu wa Jadi Simba na
Yanga ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka kila kona ya nchi hii na
nchi za jirani.
Makocha wa pande zote mbili Patrick
Phiri wa Simba na Mbrazili Marcio Maximo, kila mmoja amejitapa kuondoka na
ushindi siku hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri msimu huu.