ame
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
WAKATI Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema yuko tayari kuwaachia nyota wake kusajiliwa na klabu nyingine kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, mshambuliaji wake nyota Ame Ally Amour amesema anakaribisha ofa kutoka kwa timu nyingine zikiwamo Simba na Yanga.
Ame, aliyejiunga na Mtibwa msimu huu akitokea Chuoni FC ya Ligi Kuu ya Zanzibar, amefunga mabao manne katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), sawa na Mrundi Didier Kavumbagu wa Azam FC, Danny Mrwanda wa Polisi Morogoro na Rama Salim wa Coastal Union, jambo ambalo limewatoa udenda Simba waliotangaza nia ya kumsajili kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Akiwa mjini Unguja, Zanzibar, Ame amesema bado hajapokea ofa kutoka kwa klabu yoyote kwa nia ya kumnasa kipindi hiki cha usajili lakini yuko tayari kujiunga na timu yoyote itakayompa maslahi mazuri.
“Jambo zuri kwa Mtibwa Sugar ni kwamba hawawazuii wachezaji kusajiliwa na timu nyingine zinapowahitaji. Niko tayari kujiunga na timu yoyote itakayonipa ofa nzuri. Mpaka sasa sijazungumza na timu yoyote iwe Simba na Yanga ambazo nimekuwa nikihusishwa na baadhi ya vyombo vya habari,” amesema Ame.
Kocha Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri katika mahojiano na mtandao huu mara tu jijini Dar es Salaam, ameweka wazi baadhi ya mambo yaliyomo kwenye ripoti yake ya mechi saba zilizopita za VPL yakiwamo mapendekezo ya kuwanasa nyota wawili wa Mtibwa Sugar, Ame na beki wa kati ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina.
Mabeki wa kati wa Mtibwa Sugar ambao wameng’ara msimu huu ni Salim Mbonde, ambaye ameitwa hadi kwenye kikosi cha Taifa Stars na Andrew Vincent.
“Tuko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mipango yetu ya kuiimarisha Simba kipindi hiki cha usajili. Tumependekeza tusajili beki mwenye nguvu na mshambuliaji mmoja, na wote hawa tumepanga kuwachukua kutoka Mtibwa. Hakika timu hiyo ina wachezaji wazuri katika kila idara,” amesema Phiri.
“Tumependeza ipelekwe ofa ya kumchukua Ame na mmoja wa mabeki wa kati wa Mtibwa. Mabeki wote wa kati niliowaona katika timu hiyo wana nguvu na wanajua kukaba. Ninaamini watatufaa zaidi.
“Kama Mtibwa hawatakubaliana na sisi, basi tutaangalia nje ya mipaka ya Tanzania. Nchi ya Kenya inasifika kwa kuwa na mabeki wazuri pia, lakini kwa sasa tumeona tuanze kwa kuwaomba Mtibwa na muda wowote tutawasilisha ofa kwao kwa ajili ya wachezaji hao,” amesema zaidi Phiri.
Alipotafutwa kwa simu leo mchana kuzungumzia usajili huo, Mexime amesema hawezi kuwazuia wachezaji wake kwenda kupiga pesa katika klabu kongwe nchini, Simba na Yanga.
“Mimi sina tatizo na hilo, wakileta pesa tutapokea ili wachezaji wetu pia wanufaike. Maisha ni fedha, waache wachezaji waende Simba na Yanga kupata fedha, lakini mpaka sasa hatujapokea ofa yoyote ya mchezaji wetu kutakiwa na klabu hizo,” amesema Mexime.
Aidha, nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, amesema hana mpango wa kusajili mchezaji hata mmoja katika kipindi hiki cha dirisha dogo na endapo Simba itafanikiwa kuchukua nyota hao wawili, atapandisha wakali wengine kutoka kikosi chake cha vijana kwa kuwa “Mtibwa ina hazina kubwa ya wachezaji.”
Mtibwa Sugar inaongoza kwa kupika nyota wa soka nchini ambao wamekuwa wakisajiliwa na klabu kongwe nchini, Simba na Yanga. Baadhi yao ni makipa Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Shaban Kado (Yanga, Coastal), washambuliaji Hussein Javu na Said Bahanunzi (Yanga) na mabeki Juma Abdul (Yanga) na Issa Rashi ‘Baba Ubaya’ (Simba).
 
Top