KIPA namba mbili wa Yanga ameandika barua ya kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja uliobaki kwa uongozi wa timu hiyo huku akitaja sababu ni kukiukwa makubaliano ya mkataba huo ulio sainiwa Novemba 8 2013 wakati huo akiwa mchezaji huru.
Makubaliano yanayo lalamikiwa na Kaseja ni kutomaliziwa pesa zake za usajili milioni 20 ambazo walikubaliana na uongozi wa Yanga atalipwa kwa awamu mbili ili kukamilisha dau la milioni 40 ambazo ndiyo amesajiliwa kipa huyo akiwa kama mchezaji huru.
Kaseja amesema Novemba 8 2013 Yanga walimpa milioni 20 na kumuahidi kumpa 20 zilizobaki Januari 15 2014 na endapo makubaliano hayo hayatotekelezwa mkataba huo utakuwa umevunjika na kipa huyo atakuwa huru kuchezea timu nyingine atakayo muhitaji.
Wiki mbili zilizopita Goal iliandika habari kuhusu wakala wa Kaseja Abdulfataah Saleh,kuutaka uongozi wa Yanga kuhakikisha unamlipa mteja wake fedha hivyo vinginevyo mkataba huo utavunjika ifikapo mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa ligi ya msimu huu wa 2014/15.
Abdulfataah Salehe aliupa masharti mawili uongozi wa Yanga sharti la kwanza ni kuhakikisha unamlipa mchezaji huyo pesa zake zilizobakia ili aweze kuiendelea kuichezea timu hiyo na sharti la pili ni ikishamlipa ihakikishe inampa nafasi kwenye kikosi cha kwanza mteja wake ili kiwango chake kiendelee kuwa juu na ikishindikana mkataba huo utakuwa umevunjika.
Kati ya hivyo Yanga haija tekeleza hata agizo moja ikiwemo kumpanga kikosi cha kwanza kipa huyo kwani tangu kuanza msimu huu Kaseja hajaidakia Yanga hata mechi moja ya Ligi Kuu Tanzania bara na ameendelea kuwa chaguo la pili kwa kocha Marcio Maximo huku Deogratius Munish akiwa chaguo la kwanza.
Kutokana na hali hiyo ni vigumu kwa Kaseja kuonekana kwenye benchi la Yanga wakati ligi hiyo itakapo endelea kuanzia Desemba 26 na kuna uwezekano mkubwa kipa huyo akarudi kwenye timu yake ya zamani yenye upinzani mkubwa na Yanga ambayo ni Simba.