MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC wamedaiwa kusaka saini ya mshambuliaji wa El Merreikh na Timu ya Taifa ya Mali, Mohamed Traore baada ya kufanikiwa kumnasa beki Serge Wawa kutoka kwa mabingwa hao wa Kombe la Kagame.
“Taarifa zinazohusu usajili wa Azam ambazo bado hazijawekwa kwenye mtandao rasmi wa Azam FC si rasmi. Tukiweka kwenye mtandao wetu zitakuwa rasmi,” amesema Msemaji wa Azam FC, Jaffari Idd Maganga baada ya kutafutwa na mtandao huu jijini Dar es Salaam leo mchana kuzungumzia usajili huo.
Hata hivyo, taarifa ambazo mtandao huu umezipata kutoka ndani ya uongozi wa Azam FC zimeeleza kuwa matajiri hao wa Dar es Salaam wako mbioni kumnasa mshambuliaji huyo ili kuziba pengo litakaloachwa na mshambuliaji wao kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche ambaye yuko mbioni kutimikia Malaysia.



Tchetche, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2012/13 na mchezaji bora wa ligi hiyo msimu uliopita, yuko mbioni kujiunga na Klabu ya Kelantan ya Malaysia.
“Ndiyo kuna ofa kutoka Kelantan FC, imefika Azam FC na wanaendelea na majadiliano. ninasubiri kusikia kutoka kwao. Niko tayari kwa lolote, mimi ni mchezaji, ninaweza kucheza popote,” amesema Tchetche leo.
Aidha, mwishoni mwa wiki iliyopita, mmoja wa viongozi wa klabu moja ya Ligi Kuu ya Sudan ambayo ilikuwa inafukuzia saini ya Tchetche, alisema kuwa pacha huyo wa Michael Bolou (wa Azam FC pia) tayari ameshamalizana na klabu hiyo ya Malaysia.
“Sisi tulikuwa tunamtaka sana mchezaji huyo lakini tuymepata taarifa amekwenda Malaysia na ameshasaini mkataba na moja ya timu za huko,” alisema kiongozi huyo.

Tchetche ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa wanalambalamba, aliondoka nchini baada ya mechi yao ya Mbeya City na akakosa michezo miwili ya VPL waliyopoteza 1-0 dhidi ya JKT Ruvu na Ndanda FC huku uongozi wa Azam FC ukidai kuwa nyota huyo alikwenda kwao Ivory Coast kutatua matatizo ya kifamilia
 
Top