MBEYA City imepoteza mechi yake ya tatu mfululizo msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakani jijini Tanga leo jioni.
Magoli ya wenyeji wa mechi hiyo ambayo iliahirishwa kuchezwa jana kutokana na mvua kubwa, yamefungwa na Malimi Busungu aliyefunga kwa penalti iliyotolewa na refa Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam baada ya beki Hassan Mwasapili kumchezea rafu Nassoro Gumbo dakika 11 na Ally Nassoro aliyefunga la pili dakika ya 24 baada ya kuwatoka mabeki a Mbeya City.
Hadi mapumziko, Mbeya City inayonolewa na kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi, ilikuwa nyuma kwa magoli mawili.
Goli la kufutia machozi la wageni limefungwa na kiungo Steven Mazanda kwa krosi iliyokwenda langoni dakika 76.
Mbeya City iliyopoteza pia 1-0 nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Azam FC na Mtiba Sugar katika mechi zake zilizopita, inakamata mkia katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi tano wakati Mgambo Shooting wamekwea hadi nafasi ya sita wakiwa na pointi tisa.
Mbeya City ilianza kushika mkia katika msimamo wa ligi mara tu baada ya mechi za jana.
Wakazi wa Mbeya wamekuwa wakieleza kuwa matokeo mabovu ya timu hiyo msimu yanatokana na kuondoka kwa aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Maka Malwisi anayeinoa Panone FC ya Kilimanjaro inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL)