Na Baraka Mbolembole
Akiwa na hasira, kocha mkuu wa klabu ya soka ya Simba, Zdravko
Logarusic alilazimisha timu hiyo kurejea jijini, Dar es Salaam, mara baada ya kikosi chake kuchapwa na timu iliyokuwa mkiani, Mgambo JKT.
Viongozi wa timu hiyo walikuwa wamepanga kwenda moja kwa moja jijini, Mbeya ambako walikuwa na mchezo mwingine dhidi ya Mbeya City ili kwenda kujiweka sawa na mchezo huo uliomalizika kwa sare.
ILIMAANISHA NINI…
Akiwa na mtindo wa kubadilisha wachezaji kwa haraka, Logarusic
alitangaza mara baada ya mchezo na City kuwa anahitaji muda zaidi katika kazi yake ndani ya timu hiyo, ila akajikuta kwa mara nyingine akichapwa mabao 3-2, na JKT Ruvu, hali ambayo ilizua tafrani kubwa baada ya mashabiki kuchoshwa na matokeo hayo.
Tayari kocha huyo amefanya maamuzi kwa asilimia zaidi ya 70 kuhusu mustakabali wake klabuni hapo mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa muda mfupi (miezi sita), kama ni kuondoka au kuendelea kuwanoa mabingwa hao wa zamani ambao wamesambaratika kwa sasa.
Hakuna kitu cha shangaza katika mtindo wa ufundishaji wa kocha,
Logarusic na namna ambavyo amekuwa akiiongoza timu yake.
Simba ina matatizo makubwa, na kocha huyo awali alionekana kuyaondoa kutokana na matokeo mazuri ambayo alikuwa akiyapata wakati alipoanza kazi yake.
Kipigo katika mchezo wa fainali kutoka kwa KCC ya Uganda katika mchezo wa fainali wa michuano ya Mapinduzi, mwezi uliopita kilianza kuchochea upya mgogoro uliopo kati ya kamati ya utendaji ya klabu na mwenyekiti wao, Mh. Aden Rage.
Wale wa kamati ya utendaji walidai kuwa kitendo cha mwenyekiti kuhudhuria mchezo ule kilikuwa tatizo.Baadae wakasema kuwa timu hiyo imekuwa ikihujumiwa. Je, ni nani anayeihujumu Simba? Jibu wanalo wenyewe ila kauli ya mwenyekiti, Rage kuwa hajahafiki uwepo wa kocha Loga, kauli yake hiyo imekuwa sawa na fimbo inayomchapa yeye mwenyewe kwa wakati huu.
Hata, kocha amewahi kusema kuwa matatizo yapo katika timu na yale ya kiutawala ndiyo yanaimaliza timu hiyo kwa kuwa yamekuwa yakiingia hadi ndani ya timu na kuwaathiri.
Bado inashangaza kwa timu iliyo na wachezaji kama, Ivo Mapunda, Yaw Berko, Joseph Owino, Donald Musoti, Henry Joseph, Amis Tambwe, Uhuru Suleiman, Girbelt Kaze, Abdulhalim Humud, Jonas Mkude, na rundo la wachezaji vijana ikishindwa kupata matokeo.
Simba wamekusanya pointi mbili katika michezo minne ya hivi karibuni wakati ndiyo timu iliyocheza michezo mingi ya maandalizi kabla ya ligi kuanza.
Kosa kubwa ambalo, Logarusic amekuwa akilifanya ni kuwachezesha wacheza ambao hawamsaidii katika kazi yake. Wachezaji ambao wanaamini kuwa kocha ndiye muwajibikaji wa matokeo mabaya na si wao.
Loga, amejitahidi sana tangu aje Simba, na si yeye tu hata
watangulizi wake, Liewig na Kibadeni. Mchezaji muhimu kwake baada ya Tambwe ni wale ambao wanaonesha kujituma na kutaka kuisaidia timu.
Owino, Musoti, Mkude ni mfano mzuri kuwa kuna kundi dogo la wachezaji wanajituma na wengine wengi hawana msaada kwa timu hiyo. wapo vijana kama Ramadhani Singano, William Lucian, ambao wanaonekana kucheza kwa kujituma ila kundi la wachezaji hawa halina msaada. Uhuru, Ramadhani Chombo,
Joseph, Haruna Chanongo, Edward Christopher, Issa Rashid, Humud, wakati pia kuna kundi lingine la wachezaji linacheza katika mtindo wa kipima joto, leo wapo katika viwango vya juu na kesho wanavurunda.
Amri Kiemba ni kinara katika kundi hili, Haruna Shamte pia amekuwa mchovu japo yupo klabuni hapo kwa muda mrefu.
Ni hatma ya Simba sasa...? Kama wachezaji hao
wangekuwa wanajituma Simba ingenufaika nao, ila sasa ni mizigo mikubwa kwao kwa kuwa hawajui kwa nini wapo katika timu hiyo.
JEZI YA SIMBA NI NZITO
Si, kila mchezaji inaweza kumtosha. Huku Logarusic akitupiwa lawama kwa kutokuwa mvumilivu kwa wachezaji wanaovurunda. Ni lazima tukumbuke kuwa wengi wa wachezaji ambao
wamekuwa wakitolewa haraka uwanjani kwa kufanyiwa mabadiliko wanakuwa wanacheza kwa namna wanavyotaka wao au kwa kufuata maelekezo ya mabosi wao waliowasajili klabuni hapo.
Simba wanatakiwa kuachana na neno 'tunajenga' badala yake wawe na timu ya ushindani kila msimu. Ni uongo kusema wanajenga timu wakati wachezaji walioanzisha mradi huo wa
ujenzi wengi wameshikwa.
Wameshikwa kivi? Na nani aliyewashika?. Watu fulani ambao hawapendi kuona chama linasonga.
" Nikwambie kitu? Katika maisha chochote kinaweza kutokea. Kwa matatizo niliyokutana nayo Simba kama si nguvu za Mungu ningeshaachana na soka la Tanzania' aliwahi kuniambia mchezaji mmoja wa timu hiyo wakati alipokuwa nje ya Simba wakati huo.
Kama wachezaji wanajua matatizo yaliyopo klabuni hapo na bado anapata nafasi ya kwenda kucheza nje na anaitosa ili arejee Simba ni upuuzi.
Simba ina wachezaji wazuri na wana mradi mkubwa wa wachezaji vijana wa kuwasaidia katika misimu inayokuja, ila wapo wengine wanatakiwa kuondoshwa kwa kuwa hawajui thamani ya jezi ya Simba.
Jezi ya timu hiyo ni nzito na mchezaji ambaye anaivaa ni lazima afanye kazi kubwa ili apendeze nayo. Kina, Suleiman Matola walijituma zaidi na zaidi ili kupata mafanikio.
Hawa kina Issa ' baba ubaya' na wenzake imewashinda.Si kila mchezaji mzuri anaweza kuivaa jezi ya Simba na ikamtosha. Wale ngangari wamefanikiwa ila wale dhaifu wameshindwa. Kushindwa kwao ni matokeo ya kuingia uwanjani na maagizo kuwa leo, washinde, kesho watoe sare, na kesho kutwa wafungwe. Si, haki kwa kocha kutupiwa lawama hovyo, mchezaji anayeshindwa kufuata maagizo ya kocha wake huyo hafai.
Timu ya mwisho kufunga mabao matatu katika mchezo dhidi ya Simba ilikuwa ni Yanga, lakini JKT Ruvu nao wameweza kufanya hivyo.
Nakumbuka wakati ule Simba ikiwa nyuma ya mabao 3-0 dhidi ya Yanga aliyekuwa kocha wao, Kibadeni aliwaambia wachezaji wake kuwa; Magoli waliyokuwa wamefungwa yametosha, na alikuwa akijua kuwa kuna timu mbili kati yao. Timu ya ndani ya uwanja ( wachezaji wanaofuata maagizo yao) na timu ya nje ya uwanja ( wachezaji wanaocheza kwa kufuata maagizo ya mabosi wao).
Mwisho, Kibadeni akawaambia kuwa warudi kipindi cha pili wakacheze mpira. Simba ikakomboa mabao yote matatu, jana kiliwakuta nini?.
Wachezaji hawana uwezo ndiyo maana anakuwa akiwafanyia mabadiliko ya haraka?. Ndiyo hawaoneshi uwezo na hilo ndilo ambalo linakuwa likivuruga mipango ya Logarusic. Tatizo la Simba si kocha ni matokeo ya ubinafsi wa watu wengine wenye maslai yao binafsi na visasi vya utawala. Hili si tatizo la Rage peke yake ni la Simba wote kwa kuwa maagizo mabaya ya wachezaji yanatoka katika sehemu ya wanachama wao.
Wakati wengine wakiumizwa na matokeo hayo kuna wachezaji wanakuwa wakinufaika. Ila wana mwisho wao kwa kuwa wengi waliwahi kufanya hivyo na hawakuwahi kupata matunda yoyote mazuri.
Napenda sana kusoma kuhusu habari za wanaharakati wa zamani, Che Guevara ni mtu ambaye namuhusudu sana katika maisha yangu japo alikufa miaka mingi nyuma. Alikuwa na moyo wa kujitolea, mpambanaji wa umma, mtu mwenye huruma, na binadamu shupavu.
Marehemu Dr. Martin Luther King Jr aliwahi kusema; ' Ukimya wa rafiki yako unaumiza sana, kuliko kelele za adui yako' alikuwa na maana iliyojificha ila ipo wazi tu. Poleni, Simba vidole vyenu viondoeni kwa Loga na watazameni wachezaji wenu na mtathimini mchango wao kwa timu yenu.
Watazameni watu wenu wa karibu walio na timu ni tatizo la
kwanza. Loga ni kocha wa miezi sita tu, wala sitashangaa asipongezwa mkataba lakini anao ubora wake wa kusoma mchezaji na mchango wake.