Atakubali?: Michael Richard Wambura rufani yake imekataliwa na kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF baada ya kubainika alipiga kampeni kabla ya muda ikiwa ni mara ya pili anafanya kosa hilo. Mara ya kwanza yeye na Evans Aveva walipewa onyo kali la maandishi baada ya kumwaga sera siku ya kuchukua na kurudisha fomu.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana jana (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.
Kwa namna moja ama nyingine suala hili limegusa hisia za baadhi ya wanachama wa Simba hususani wenye mapenzi na Michael Wambura.
Baadhi ya wanachama wa Simba walikuwa wanampigania Wambura ili agombee urais na hii ilidhihirika wakati ule alipoenguliwa na kamati ya uchaguzi ya Simba sc. Mengi yalizungumzwa, lakini mgombea huyu alikata rufani na kushinda na hatimaye kurudishwa katika mchakato wa uchaguzi.
Kabla ya kupeleka Rufani yake TFF, Wambura alikutana na waandishi wa habari na kueleza kutoridhishwa na maamuzi ya kamati ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wake, Wakili Dkt. Damas Daniel Ndumbaro na kusema anakata rufaa kupinga.
Kweli alikata rufaa na kurejeshwa kwenye uchaguzi. Kwa wanaomuunga mkono Wambura ilikuwa furaha kwao kuona anaendelea kuwania Urais. Kwa wanaompinga pengine ilikuwa pigo kwao.
Pande zote mbili zilitambiana hususani wa upande wa Wambura. Kwa bahati mbaya sana, mgombea baada ya kurudishwa na kamati ya rufani ya uchaguzi ya TFF alikutana na waandishi wa habari na kuelezea furaha yake ya ushindi.
Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi (kushoto) alisema jana suala la uchaguzi wa Simba litapatiwa ufumbuzi na akapongeza juhudi za Aden Rage kuwasiliana kwa ukaribu na shirikisho, kauli iliyoonekana kuwawashia Simba taa ya kijani
Lakini sijui ni kujisahau au ni kuzidi kwa furaha, wakati namsikiliza Wambura siku ile, alitamka maneno ambayo binafsi nilihisi yatahusishwa na kampeni. Ni maneno ambayo hayakustahili siku ile, nilijua Wambura ataeleza tu furaha yake ya kushinda, na kusema anasubiri muda wa kampeni ufike.
Kabla ya hapo, Wambura na Aveva walishapewa onyo kali baada ya kupiga kampeni siku ya kuchukua na kurudisha fomu. Aveva amekuwa mjanja kwani toka siku hiyo hajasikika tena, zaidi ya watu wanaosemekana kumuunga mkono, wakitajwa `Friends of Simba`.
Nilitegemea Wambura kuwa mtulivu baada ya kushinda Rufani, sijui marafiki zake walimshauri nini. Lakini kilichoonekana ni kutaka kupambana na Azim Dewji ambaye kabla alimponda Wambura na kusema hafai kuwa Rais wa Simba kwasababu hataki wafadhili.
Azim sio mgombea na kwa bahati Mbaya katiba ya Simba ina mapungufu kwa hili, haina namna ya kumbana mwanachama anayepiga kampeni kabla ya muda, Hata katibu wa kamati ya uchaguzi ya Simba, Khalid Kamguna alikiri mapungufu haya na kusema watawashauri viongozi wajao wafanyia marekebisho katiba na kuingiza kipengele cha kumbana mwanachama kama Azim mara atakapoongea maneno kama yake wakati kampeni bado.
Wambura alistahili kupima upepo kwasababu kamati ya uchaguzi ya Simba ina mtu mfuatiliaji kama Ndumbaro. Namjua wakili huyu kwasababu amenifundisha somo la `media Law` chuo kikuu cha Dar es salaam. Ni mtu mwenye msimamo na anatumia sana sheria kuamua mambo yake. Nilijua suala la Wambura atalichukulia kwa uzito na kumfuatilia nyendo zake kama mwenyekiti wa kamati.
Baada ya Wambura kushinda rufani, Ndumbaro hakusema chochote, lakini aliendelea kumfuatilia na kama alijua udhaifu wa Wambura ni katika kuzungumza mambo bila kuzingatia wakati. Simsemi vibaya, lakini alihitaji kuwa mtulivu ili kukwepa mitego ya kamati ya uchaguzi ya Simba.
Kamati ya Rufani ya TFF inayoongozwa na mwenyekiti wake, Wakili Julius Mutabazi Luzaziya (kushoto) imeamua kukataa rufani ya Michael Wambura, japokuwa wakili Lugaziya hakuwepo jana.
Kwa bahati mbaya, Wambura akajikoroga wakati anamjibu Azim. Kosa hilo limesababisha kiama chake hapo jana baada ya kuondoshwa kwa kosa la kupiga kampeni kabla ya muda, na safari hii sio kuipeleka Simba mahakami na kusimamishwa uanachama.
Kigingi hicho alikwepa, lakini akajisahau na kujichinja mwenyewe. Sidhani kama kamati ya Rufani imeogopa, naamini kanuni zimetumika na binafsi nilitegemea matokeo ya hivyo.
Haya yameshatokea, jambo la msingi ni Simba kufanya uchaguzi wao. Kwa siku mbili zilizopita nimeandika kuwa hakuna jinsi ya kuzuia uchaguzi wa Simba kutokana na mazingira halisi.
Simba inatakiwa kupata viongozi ili isajili wachezaji kwa ajili ya ligi kuu msimu ujao. Kuchelewesha uchaguzi ni kuiumiza klabu. Hata maamuzi ya Rais, Jamal Malinzi kusimamisha uchaguzi sikuyaunga mkono hata kama alikuwa na mamlaka.
Nilisema Kwamba, Malinzi alihitaji busara kuisaidia Simba kufanya uchaguzi, na kwa bahati nzuri yeye ni muungwana, jana alionesha dhahiri ameshakubali uchaguzi ufanyike na ndio maana aliruhusu kamati ya Rufani ya uchaguzi isikilize rufaa ya Wambura.
Jambo la msingi ni wanachama kupiga kura juni 29. Wambura kama atabahatika kusoma makala hii, ushauri wa bure ni kukubali kilichotokea kama kweli ana mapenzi na Simba na anataka kuiona inafanikiwa msimu ujao.
Akiamua kupambana tena kwa kuona ameonewa, mwisho wa siku, klabu yake anayoipenda itaharibikiwa. Nina amini bado ana mawazo na mchango mkubwa kwa klabu. Haitakuwa dhambi kuendelea kutoa mchango wake hata akiwa nje ya uongozi.
Sidhani kama kiongozi pekee ndiye anaweza kuisaidia klabu. Japokuwa ni kweli kuwa lazima awepo mtu wa kuwaongoza wenzake, lakini naamini Wambura asukumwe na busara ili aache uchaguzi ufanyike na maisha mengine yaendelee.
Michael Richard Wambura, yawezekana hajapenda na kukubaliana na maamuzi ya kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF, lakini kumbuka hao hao ndio walikupa ushindi kwasababu waliona una haki.
Hao hao wamekuondoa kwa mara ya pili baada ya kugundua una makosa. Ni busara kukaa pembeni kuliko kuendeleza sinema hii ambayo unaweza kulaumiwa na wanasimba wengi mara mambo yatakapokuwa mabaya.
Wanachama wanaompenda Wambura, kumbukeni kuna kushinda na kushindwa. Mlishinda mara ya kwanza, wenzenu wakaumia. Sasa wao wameshinda, waacheni waendelee na uchaguzi na ninyi nendeni mkachague. Hakuna haja ya kususia uchaguzi eti kwasababu mnayempenda kaondolewa.
Simba ni yenu wala sio ya Wambura wala Aveva wala Tupa. Mkigombana kwasababu ya wagombea, haitawasaidia kuijenga klabu. Mgombea mmoja ameondoshwa, angalieni waliobaki, mtakayemuona anafaa mchagueni kwa manufaa ya klabu yenu.
Kila la kheri Simba sc katika uchaguzi wenu.