UNAJUA kwamba Ruvu Shooting ndiyo timu ya mwisho kufungwa na Simba
katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) katika miezi nane
iliyopita? TEGA SIKIO…
Mara ya mwisho Simba kuibuka na ushindi VPL ni pale ilipoifunga Ruvu
Shooting mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam msimu
uliopita, ndipo bundi akaingia na kuanza kuitafuna klabu hiyo uwanjani
hadi leo.
Ikumbukwe kuwa Simba iliyolazimika kuwatimua makocha wake Abdallah
‘King’ Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ mara tu baada
ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa VPL msimu uliopita, kikosi
kikiwa nafasi ya nne nyuma ya Yanga, Azam na Mbeya City, Simba ilishinda
mechi tatu tu mzunguko wa pili ikiwa chini ya waajiriwa wapya, Mcroatia
Zdravko Logarusic na msaidizi wake Selweman Matola.
Simba ilizishinda Rhino Rangers, JKT Oljoro iliyoshuka daraja na Ruvu Shooting ya kocha Mkenya Tom Alex Olaba.
Baada ya hapo Simba ilifungwa na Mgambo Shooting, Azam FC, JKT Ruvu,
Ashanti United iliyoshuka daraja na Coastal Union huku ikitoka sare na
Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Tanzania Prisons na Yanga.
Msimu huu Simba imecheza mechi sita za VPL, zote ikiambulia sare, 2-2
nyumbani dhidi ya Coastal Union, Polisi Morogoro, Stand United na suluhu
dhidi ya Yanga kabla ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na 1-1 vinara wa
msimamo Mtibwa Sugar.
Simba vs Ruvu Shooting msimu uliopita
Kwa kifupi, Simba imecheza mechi 12 za VPL bila ushindi baada ya
kuwafunga 3-2 ‘maafande’ wa Ruvu Shooting miezi nane iliyopita. Je,
itaanza kupata ushindi dhidi ya timu hiyo ya Pwani Jumapili na kuondoa
gundu la sare?
Tayari uongozi wa Ruvu Shooting kupitia kwa msemaji wa klabu hiyo, Masau
Bwire umewweka wazi kuwa hauko tayari kuona timu yake inatumika
kumaliza gundu hilo linaloukabili uongozi wa Simba chini ya Rais wake,
Evans Aveva ambaye sera yake ya pointi 3 magoli 3 inaonekana kufeli.
“Tumesikia wamempa kocha wao (Mzambia Patrick Phiri) mechi mbili ikiwamo
yetu kwamba lazima ashinde vinginevyo wanamtimua. Tunachoweza kumshauri
Phiri ni kwamba akate tiketi mapema na kutanguliza mabegi na vifaa
vyake uwanja wa ndege maana sharti hilo ni gumu mno mbele ya Ruvu
Shooting,” anasema Bwire.
Lakini, Aveva amekaririwa leo na magazeti makubwa nchini akieleza kuwa
wametengua sharti lao kwa benchi la ufundi baada ya kubaini kuna
matatizo mengine ndani ya timu yao.
Simba baada ya kuambulia sare sita mfululizo msimu huu, tayari
inaonekana kuvurugana baada ya kuwasimamisha viungo wake Amri Kiemba na
Shaban Kisiga pamoja na winga Haroun Chanongo kwa madai ya utovu wa
nidhamu na kucheza chini ya kiwango.
Timu hiyo ya msimbazi inakutana na kikosi cha kocha Olaba, Ruvu Shooting
ambacho kimepoteza ugenini 1-0 mechi yake iliyopita dhidi ya mabingwa
wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga Jumamosi.
Ruvu Shooting pia imeuanza vibaya baada ya kupoteza mechi zake mbili za
mwanzo 2-0 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons na 2-0 ugenini dhidi ya
Azam FC kabla ya kutoka suluhu nyumbani dhidi ya Mbeya City, ikashinda
3-1 ugenini dhidi ya Ndanda FC, ikashinda 1-0 nyumbani dhidi ya Polisi
Morogoro kabla ya kupoteza Jumamosi.
Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia
Kitengo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), inakamata nafasi ya saba ikiwa
na pointi saba. Imefunga magoli manne huku ikiruhusu nyavu zake
kutikishwa mara sita wakati Simba iko nafasi ya tisa ikiwa na pointi
sita, imefunga magoli sita na kufungwa sita pia.
Mechi nyingine za mwishoni mwa wiki zitawakutanisha vinara wa msimamo,
Mtibwa Sugar dhidi ya ‘ndugu zao’ Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu,
Turiani km 100 kutoka mjini Morogoro, Stand United wataialika timu
iliyo mkiani baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, Mbeya City kwenye
Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga wakati JKT Ruvu iliyofunga 2-1
na Polisi Morogoro Jumamosi, itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja
wa Azam.
Yanga watakuwa waliorejea baada ya kupigwa 1-0 na Kagera Sugar wakiwa
Kanda ya Ziwa, watawakaribisha Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa
Jumamosi, Tanzania Prisons watakuwa wageni wa Polisi Morogoro kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati mabingwa watetezi Azam FC, baada
ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu (nyumbani) na
Ndanda FC (ugenini), watakuwa wenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wao
wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam Jumamosi.